Wednesday, July 18, 2012

Z A N Z I B A R, Z A N Z I B A R !!!







Inna lillahi Alaa, waina illahi rajiuuni,

Visiwani tunalia, kwa kukosa tumaini,

Kila siku kufiliwa, kwenye njia baharini,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Ajali tumezoea, sera mpya twazibuni,

Kwa ajizi na udhia, nchi wamesharubuni,

Wenye fedha waachiwa, leseni za mumiani,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Ndugu ninawalilia, inaniuma moyoni,

Pole yao nakataa, naona kama uhuni,

Tunaweza kuzuia, amini usiamini,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Eti meli zatembea, ofisi hatuzioni,

Au ni za Liberia, au kutoka Japani,

Seagull yaelea, wenye mali kina nani?

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Mitumba twaitumbua, nayo yatufanyanini?

Ndiyo sera na sheria, kukwaa na kujihini,

Kuna watu wachangia, twamsingizia shetani ?

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



La bidanamu kavaa, huyo jini mumiani,

Na uhuru amepewa, kuufanya uhaini,

Ndani nje kuchungua, yasifichwe asilani,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Fidia zetu nazaa, zinatushusha thamani,

Ndio ma'na inakuwa, wanakosa umakini,

Kitu kidogo wakiipewa, twaumia masikini,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !



Jalali twakulilia, kwa adha na usononi,

Ndiye uliyebakia, viumbe wavithamini,

Tulioishawachagua, wametuacha mataani,

Zanzibar, Zanzibar, kila siku tunalia !





No comments: