Saturday, May 5, 2012

Wanafiki mtaona



Mnafiki hufurahia, mwenzie akiumia,
Moyoni huzawadiwa, roho mbaya kujaliwa,
Kufa ukatarajia, yeye hakuandikiwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Mapema walitakiwa, salama kuzingatia,
Wao wakayaachia, hadi kwingia pabaya,
Kama mamba watatoa, machozi maji yalojaa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Taifa wanaligawa, kwa wanayokusudia,
Njia hawajaijua, wameanza kutembea,
Mashimoni kuingia, nani atawashangaa?
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Porini wataingia, msitu hawajaujua,
Swala anapotokea, duma watamdhaia,
Na wakianza kukimbia, mbio hawatamfikia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Moshi wanaukimbia, kumbe motoni waingia,
Macho hawakufungua, nini utatarajia,
Kazi yao kuambiwa, wakabaki itikia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Madhambini wawatia, hata sffi walokuwa,
Uongo wakaujua, kwalo wakabarikiwa,
Kama si kulaaniwa, kama ninavyoelewa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Kuiba waumbuliwa, ujanja wapakuliwa,
Chungu kinachobakia, halali kimebakia,
Imetamka dunia, mwisho unakaribia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Maneno kuitikiwa, zamani ilikuwa,
Sasa vitu vyatakiwa, machoni tukavitia,
Midomo mngeshonea, kwa sindano na shazia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wazo likishazaliwa, ni vigumu kuliua,
Mwaweza watu kuua, ila wazo labakia,
Na kila ukizuia, ndivyo linavyochanua,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wakati ukifikia, liwalo lazima kuwa,
Hakuna wa kuzuia, hatangani angekuwa,
Jaribu utaumia, ukabakia kulia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Ukuta ninawaambia, ndivyo wakati huzua,
Na usiyotarajia, konkreti huja kuwa,
Na ngumi ukiitia, kuvunjika waridhia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Nchi inatakiwa, ushindani kuulea,
Wachungu wawili kuwa, au zaidi yafaa,
Na nyote kupigania, ya haki yaliyokuwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Ukitaka ng'ang'ania, utamu kuukamia,
Rahisi haitokuwa, uchungu kuukataa,
Hakuna aliyezaliwa, kutawala kajaliwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Nusu kura wakataa, hamuoni ni udhia,
Sababu hamjajua, na gamba hamjavua,
Uoza mnatumiwa, na hayo ndiyo maua,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wakati umewadia, fakiri kuangalia,
Nao pia ni wazawa, na fursa walilia,
Wenyewe kujichagua, pabaya mtaingia,   
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wagonjwa twawaombea, Mola kuwaangalia,
Maumivu kupungua, na nafuu kuijua,
Afu tunakulilia, na haki kuangalia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wa kawaida raia, hospitali watakiwa,
Kuwaonyesha wakiwa,  upendo uliojaa,
Wakubwa wakikataa, bora zaidi itakuwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!


No comments: