Saturday, May 5, 2012

Dawa dua na kufunga



MOLA tukimgeukia, huwa yasiyowaziwa,
Na wanaojipangia, yao yakapanguliwa,
Inahuu yakidunaa, waakidu kaydaa,
Dawa dua na kufunga, viongozi mafisadi !

Mbali ninaangalia, hakuna lilo sawia,
Arijojo nahofia, ndio tunakoelekea,
Upepo umepungua,  nguvu wajikusanyia,
Dawa dua na kufunga, wabunge wanaohonga !

Kiumbe hatoitoa, nusura ninayoijua,
Uwezo wameishiwa, si watu wa kujaliwa,
Toba wameikataa, nia zao kutimia,
Dawa dua na kufunga, mahakimu wadhalimu !

Shiriki wanakazia, njoo jua, toka jua,
Tambiko kuabudia, nazo taslima pia,
Wengi wameshapotea, nasi tunajionea,
Dawa dua na kufunga, wanasiasa waovu !

Dini wazikatalia, ibada kuzingatia,
Shere wakawafanyia, wanaowaaminia,
Wajinga wakadhania, rahisi kuwahadaa,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

Nafusi zawahadaa, katika hii dunia,
Bora wanajidhania, viumbe wa kuzaliwa,
Mifupa wajaokuwa, muongo haujaishia,
Dawa dua na kufunga, viongozi mafisadi !

Dhamana waitibua, na uongo kutumia,
Heri wanaikataa, moto kujipalilia,
Siku zinahesabiwa, na wao hawajajua,
Dawa dua na kufunga, wabunge wanaohonga !

Waja ninawaambia, ni kufunga nazo dua,
Ndio sasa zatakiwa, maamuzi kuamua,
Aachiwe wa kuachiwa, kitu asiyekosea,
Dawa dua na kufunga, mahakimu wadhalimu !

Naapa tukimrudia, tena hatutapotea,
Tawba ataitoa, na nuru kutujalia,
Iwe njia twaijua, si wao kufuatia,
Dawa dua na kufunga, wanasiasa waovu !

Na wanaonunuliwa, hao wameishapotea,
Duania waidhania,  ndio bora ilokuwa,
Kumbe mkenge waingia, kwani hawajajitambua,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

Ninamaliza kwa dua, kumwangukia Jalia,
Na sujuda kuitia, chini nikanyenyekea,
Hatuna pakukimbilia, ila kwake kurejea,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

No comments: