Saturday, June 12, 2010

Hili halina maneno, wahenga wameafiki,
Ya nini mabishano, na hiyo mikikimikiki,
Muungwana si maneno, bali vitendo lukuki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Wataka ufungamano, bila kweli wadhihaki,
Kujenga mshikamano, watendee watu haki,
Waswihi maridhiano, basi mwogope Razaki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Kizazi hiki maono, gizani hakikaliki,
Twahoji mtafutano, na kulea wanafiki,
Twalitaka tangamano, hatutaki mamluki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Fanyeni mahojiano, na mengine mhakiki,
Hili la maelewano, dai letu, yetu haki,
Ni udhaifu utengano,milele hatuutaki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Umeisha mchuano, vizingiti na visiki,
Yatajiri mapatano, na mseto kuafiki,
Uongozi mlingano, lengo letu la twariki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Fursa zetu mshono, lakini nyuma twabaki,
Kichinichini mapigano, wengine wanatuhiliki,
Haishi misiguano, nchi haitajiriki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Farouk nawe Machano,vingine hatuimariki,
Tushikaneni mikono, na Mola atatubariki,
Mradi maelewano, tutahimili mikiki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Hatukulala kipono, kuwa tena hatuamki,
Tumeona mabishano, na njia isiyo milki,
Na ukweli ni uwiano, wananchi wastahiki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

No comments: