Saturday, June 12, 2010

Fukwe ni za wenye nacho

Masikini hana chake, fukwe sio tena yake,
Sasa fensi usivuke, pembe zote waeleke,
Kama mwana, mtu chake, asiye na fedha lwake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Pwani mshikemshike,wapi kwao kukalike,
Tokea watu wazuke, na wengine wazuzuke,
Mme hamjui mke, na dada hana kakake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Yabaki tumemetuke, wengine wangangaduke,
Kiunga chako ni chake, akiingia utoke,
Usingojee mateke, labda haki iamke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Toka haki ibweteke, na virongosi wafoke,
Dhuluma iheshimike, na mabavu yajengeke,
Sera sasa teketeke, na mjai yawa mvuke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Mnyonge na anyongeke, tajiri atajirike,
Na asiyeko muweke, aliyemo abweke,
Sautiye ikauke, na mwishowe mmzike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kwa vipi waabudike, viumbe wala matoke,
Iweje waheshimike, vibaka kamavibweke,
Na lini tuneemeke, hali mali zisanzuke?
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Na ardhi itoweke, mikononi itutoke,
Wapi mbavu tuziweke, ijapo tupumzike,
Wapi pakanyagike,mabalaa tuyavuke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Ni haki tukereheke, mnyonge hana mwenzake,
Ni wapi avumilike, apate kilicho chake,
Na lini asalimike, asetiri moyo wake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Mnyonge kabaki peke, uchumi tena si wake,
Mwache mlozi acheke,dhiki ni nafuu kwake,
Wacha hasidi wawike, uovu unawirike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kindakindaki mdeke, wenye nchi muezeke,
Vigae visigawike, na bati lisibwatuke,
Mvi zingekuwa mbwike, tungetaka tuzeeke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kijigijii msuke, twafumua mfutike,
Pekupeku msivuke, miiba isije wateke,
Mchanga sichanganyike, hapa sikwetu msinizike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Sokomoko msitake, virungu msidundike,
Eleka mwana ueleke, kizazi chenu sio chake,
Chekeni wajinga mcheke, mwacheni anufaike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

No comments: