Thursday, April 26, 2012

Msiba tulio nao



Tunalia Tanzania, msiba umeingia,
Nchi sasa inaliwa, nzige wameshaingia,
Hakuna kinachobakia, jangwa yote imekua,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Wenye meno wanajaa, hadi mifupa watwaa,
Kazi ni kujitafunia, na sio kuhudumia,
Huliwa kisicholiwa, haramu hawajaijua,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Kwa ukubwa kuupewa, leseni wamechukua,
Halali imeshakua, hata wizi kutumia,
Haraka wapigania, kileleni kwenda kaa,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Ubepari ninalia, nchi umeshaiumbua,
Haya zimetukataa, ni aibu zinajaa,
Kila ukiangalia, nusura sijaijua,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Vijana waliokuwa, tayari mabilionea,
Njia walizotumia, zote mashaka zajaa,
Na wakubwa wanajua, sijui wamegaiwa?
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Wenzangu Watanzania, ni wote tunaumia,
Daima nanyi nitakua, haki yetu kutetea,
Moto tukiwaashia, kuzimwa haitakuwa,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Shetani keshawaingia, nchi hawataifaa,
Yao wajitafutia, wao na zao jamaa,
Sasa kilichobakia, ni fatwah kujaitoa,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Na laana kuwaachia, wao na vizazi vyao pia,
Pasiwe watapotia, mguu salama wakawa,
Na kikubwa kinachokuwa, kidogo kikaishia,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Uchungu wasiokuwa, uzazi hawajaujua,
Miioyo iliyovia, yabisi imeshajaa,
Hakuna kutumainia, zuri kuja kutokea,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Yarabi nakulilia, watu wangu wapotea,
Ni usiku umekua, na hawaioni njia,
Tushushie zako taa, nuru kutuangazia,
Msiba tulio nao, ni msiba wa taifa !

Al-jumaa 27-04-2012
Zanzibar. Tanzania.

No comments: