Thursday, April 26, 2012

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Kuliko ya mtu kwetu Afrika,
Vijana wetu wananiambia,
Nao ujumbe umekwishafika!

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Ni nini walichokifikiria;
Hadi kama hayo wametamka ?
Udhia uongozi ulokuwa ?

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Lazima na mimi kuulizia,
Majibu yangu si ya uhakika,
Ila kuna walakini ninajua !

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Vipimo vipya ukivitumia,
Kila kitu sasa kinatupwaya,
Bado vya watoto tunavivaa?

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Na kusoma yawe yaeleweka,
Wengi wetu hatujajitambua,
Uvivu watu umetujaa!

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Ng'ombe huko anatunzika,
Na virutubisho pia  hupewa,
Kwa ubora nyumba zinajengeka!

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Hospitalini atibika,
Kwenye gari pekee anakaa,
Wala hakuna kudhulumika!

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Afrika hayatofanyika,
Umasikini waupalilia,
Hili ndilo bara la wastahika !

Heri kuzaliwa ng'ombe Ulaya,
Hili ndilo bara la wastahika !
Tayari waliokwishakupotea,
Na safari wala haijaanzika!


No comments: