Thursday, April 26, 2012

Siasa si kila kitu



WENGINE wamgechanua, katika teknolojia,
Na sayansi kuikwea,  kileleni kufikia,
Na biashara kupaa, hadi angani kwelea,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Kama wenu walilia, kura kwenda kugombea,
Wetu bado waotea, mataifa kuingia,
Dunia ikawajua, wala sio Tanzania,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Mbali wanafikiria, ndio mana wazamia,
Meli wasizozijua, wapi zinaeleka,
Malengo wafukuzia, waachane na udhia,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Hata soka walilia, majuu kwenda kukaa,
Timu ndogo kuchezea, mbali sana wangekua,
Na mateja na vichaa, hata nao wangepungua,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Wangali wanatakiwa, matunda kuyatungua,
Rahisi ingelikuwa, saa hizi wangetoa,
Nyumba kujijengea, ambazo tunawatania,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Sera inazikataa, mwisho zitakubaliwa,
Unafiki ulokuwa, hadithi ikatimia,
Mbichi zile zimekuwa, kumbe huku zatakiwa,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Namimi nitarudia, hadi watu wakajua,
Ukweli ulokuwa, na wakweli walokuwa,
Na kisha kujipandia, kile kinachotakiwa,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Kuna kazi kuamua, kidogo kuwagawia,
Na senti ikichangiwa, wakati wa kujitolea,
Vitatengezwa vifaa, na miji ikachanua,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Akili zinatakiwa, watu wanazifukia,
Barabara zingefaa,mwanzo hadi akheria,
Maji tungelichimbua, kila kona Taznaia,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Ila tunavyotambua, wengi watajiumbua,
Misaada wangojea, kwenda kujipaulia,
Ujasiriamalia, ndio unakataliwa,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Tunaweza jifanyia, mengi sana yalokuwa,
Ila hili wahofia, ufakiri utatoa,
Watu wakiendelea, wakubwa watang'olewa,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Uchumi wanauua, ila yao kutimia,
Kisha wanasingizia, hata vile visokuwa,
Wajinga wakiwajua, ni nini kitatembea?
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !

Mimi ninayahofia, wala sitaki kisia,
Ingawa ninayajua, na roho inaumia,
Sihiri ninakataa, kwenda kuitazamia,
Siasa si kila kitu, ila fursa hakuna !


No comments: