Thursday, April 26, 2012

Mwizi akikurupushwa

WATU ninawausia, hadhari kuichukua,
Mwizi ukinyemelea, ni vyema kujiandaa,
Kwani akishtukia, aweza akakuua,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Aibapo katulia, mipango kujatimia,
Kuta atazibomoa, na mwanya kujipatia,
Mlango akachagua, wapi pa kuingilia,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Dirisha hulichagua, ikibidi hivyo kuwa,
Ndani akatumbukia, chake kuichagulia,
Na kisha kuyoyomea, aende kujiuzia,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Ndani anapoingia, kaziye kujifanyia,
Ukaja kumshtua, uoga utamwigia,
Katika kujiokoa, kama chui atakuwa,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Aweza kukurukia, kisha akakuparua,
Ukali ukizidia, lazima atakurarua,
Na damu akakutoa, uhai kuutishia,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Ila ukijiandaa, akashindwa jitetea,
Akasalimu sheria, na mikono kunyanyua,
Pingu ukishamtia, hana la kuambulia,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Hirizi atabetua, na hata akaing'oa,
Kinga imemkataa, tena haitomfaa,
Mwenye akajijutia, watu wengi kumjua,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Itamjua dunia, na heshima kupotea,
Ukutani kuishia, mbio alizokimbia,
Na wengine huzimia, au presha kupaa,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

Hii ndiyo Tanzania, wenyewe tunajijua,
Kila mwenye kudhania, huenda akajifaa,
Huja akajaishia, chini kuja kuhcimbiwa,
Mwizi akikurupushwa, huwa mkali kama chui !

No comments: