Thursday, April 26, 2012

Milionea tungekuwa

Ndio wanaochochea, uroho nayo tamaa,
Kama mvuvi kuvua, bila nyavu kutumia,
Na kulima asojua, akavuna na kupaa,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Vijana wawahadaa, tena kisaikolojia,
Kamari imeshakua, jina lake inafaa,
Na wakubwa walokuwa, nuksi hawajaijua,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Imani zatuvunjia, na vijana kupotea,
Na vichaa walokuwa, kazi wanazikimbia,
Na idadi tunajua, mia haitafikia,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Matangazo ni balaa, tivii na redio pia,
Ovyo zinavyotumiwa, ni ila imeingia,
Na kula anayejua, wana atawaambia,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Vilio zitatutia, pasiwe pa kukimbilia,
Wanyonge tunanyolewa, kidogo tulichopewa,
Na wkubwa wanajaa, matumbo kuwalegea,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Uhuni umeingia, kucheza nazo ruia,
Na rahisi walokuwa, vijana wahusudiwa,
Ujinga waliojaa, ktuokana nayo njaa,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Milionea tungekuwa, kama hivyo ingekuwa,
Rahisi kujichumia, pale usipopandia,
Hata mie ningekuwa,  iwe ninawaringia,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Walakini haijawa, na wala haitakuwa,
Kuchuma ni kuumia, tena sana kukimbia,
Uchumi ni kukataa, mfukoni kuzitoa,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Uchumi ni kukataa, mfukoni kuzitoa,
Ila ikiwa yafaa, kwa  hivyo kuingizia,
Vinginevyo wafulia, ovyoovyo kutumia,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

Simu zinatuibia, hili ninawaambia,
Na nyie msiojua, zaidi mtaumia,
Ukiziona kimbia, salama utaijua,
Tungekuwa milionea, watu wote, kama ndivyo !

No comments: