Tuesday, April 19, 2011

Tsunami ya siasa

Tushukuru ikipita, tsunami ya siasa,
Maisha sasa ni vita,fisadi wametuposa,
Sinema wameileta, uchumi kisa mkasa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Gharika ndani yapeta, hai ni wanasiasa,
Ni maiti tunaoteta, hali zetu kwasakwasa,
Maji yanatuburuta, ni wapi yatatutosa?

Miaka iso mafuta, ngozi huwezi zigusa,
Zakatika ukivuta, ukurutu unavyotesa,
Umaskini unanata, ndiyo ya kwetu fursa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Ahadi mbawa zaota, tuna adui wa visa,
Wakubwa wazidi peta, kwa tozo pia nazo hisa,
Fukara afurukuta,macho abaki pepesa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Tsunami yatupata, Tanzania yatutesa,
Si ya Mungu kuleta, bali ni wanasiasa,
Kila kitu wamechota, bado tu sala na misa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Udini waupatkata, wa Amadi naye Issa,
Petroli waileta, chumbani wesha itosa,
Wananchi wanatweta, hawajui yanayopasa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Uongozi kuupata, si kazi kwenye siasa,
Ila vigumu kupata, ustawi na hamasa,
Subira budi kuvuta, na dua kutozisusa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

Haina kitu hii kata, moyoni ninajiasa,
Rabuka naye kuteta, afueni kutugusa,
Watu bora kuwapata, nchi ipate msasa,
Tsunami ya siasa, tushukuru ikipita.

No comments: