Tuesday, May 29, 2012

Ishi na sisi tuishi



Namtaraji Munshi, kalamu kuwa aushi,
Niyaandike bilashi, yaliyochorwa nakshi,
Iwe yangu bakshishi, kwa wajao waandishi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi sisi tufe !

Uongozi si mazishi, si kikomo cha kuishi,
Kwangu ni uanzilshi, uhai wenye najashi,
Wakubwa ni matarishi, lingine hawafikishi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi ili tufe !

Uongozi ushawishi, kama yalivyo marashi,
Nzi haukaribishi, ili kisicho tapishi,
Na mema hujaa pishi, na watu hawabakishi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi sisi tufe !

Haya ni utamanishi, kuyabeba kwa furushi,
Watu wapate bashashi, mazuri kuyanakishi,
Muda uwe hautoshi, katika wenu uashi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi ili tufe !

Mikono haurefushi, na miguu haiwashi,
Ukenda kwenye ushashi, uongo nao uzushi,
Ukawa ni hatarishi, kwa raia na majeshi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi sisi tufe !

Ni kama mama mpishi, kaziye haimchoshi,
Hupika kila mapishi, na hakika si mbishi,
Na kitu hakibakishi, hulala njaa mcheshi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi ili tufe !

Hili haumfundishi, kazaliwa nayo pishi,
Mkononi ana dishi, na jengine haumpashi,
Kaumbiwa bishaushi, hadi siku ya mazishi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi sisi tufe !

Usingojee kuishi, baada yetu mazishi,
Yakanushe matamshi, tena bila tashwishi,
Hukugeuza uzushi, na kitu haurefushi,
Ishi na sisi tuishi, usiishi ili tufe !

Atajua Kingereza ?




AJABU ilokuwa, ni wale wasiojua,
Ndio wanaopigania, Kingereza kutuoa,
Hali kukitumia utacheka na kulia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Ilmu aliyopewa, mizizi haikupewa,
Sarufi kaitungua, kichwani haijakaa,
Na anachoongea, mwenyewe anakijua,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Maudhui huchafua, upukutike mkaa,
Na majivu kuingia, kama kuni katumia,
Wala  hutomuelewa, si chake akililia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Kiutu amefulia,na asili kaishiwa,
Na huyu kuendelea, na ije  miaka mia,
Na bado ninakwambia, hapohapo atabakia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Hawa mbona nawajua,  katika hii dunia,
Walikuwepo India, hadi wakasanzuliwa,
Na Wahindi watumia, yao iliyojaliwa,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Hawa mbona nawajua, misaada walilia,
Na kila wanpoishiwa, rahisi kuzainiwa,
Lugha wakaichezea, kumbe ndio wanatuua,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Mwanzoni sikuwajua, hadi Makwetta kutua,
Mbeya nilipoingia, mjini kanitambua,
Akanipa historia, uongo nikaujua,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Kofia namvulia, ijapo kasahuliwa,
Shahidi kajipatia, yenyewe historia,
Labda waje kutia, uongo kusingizia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Watu wa kuangalia, ishara hawajajua,
Nyuma wanaelekea, hali mbele tunatakiwa,
Huu mkubwa udhia, laiti wangelijua ?
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

India nashangilia, lugha yao kutumia,
Na wenzetu wa Korea, nyuma hawajabika,
Kadhalika Malaysia, na jirani Indonesia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Vietnam nao pia, wajua yao dunia,
Filipino watambua, waukataa mzaha,
China ilitangulia, matunda yajivunia,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Kote ukiangalia, Afrika mtajua,
Lugha wanaotumia, isiyo yao ikawa,
Nadra kuendelea, tazameni Nigeriqa,
Hakijui Kiswahili, atajua Kingereza ?
Si mbwembwe na ubishhoo, na hana anachoweza?

Uongozi muflisi




Kila mtu akubali, kufilisika kubaya,
Ila ni kubwa ajali, viongozi kuishiwa,
Na ikawa afadhali, bora tu waliokuwa,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Hakuna yake mithili, viongozi kuishiwa,
Pakawepo idhiliali, hali watu kutojua,
Na Muumba kawa bahili, hataki tusaidia,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Zikabakia kauli, kila pahala zajaa,
Na vitendo ni muhali, maofisini wakaa,
Ikadhoofu hali, kwa dawa kutoijua,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Kakasirika Jalali, kwa maudhi yalojaa,
Watu wanyonga ukweli, na haki waiinunua,
Taabani binhali, ni nani mtamlilia?
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Watu wameacha sali, vimisi wafatilia,
Hiyo kwao ni asali, katika hii dunia,
Walikuwepo rijali, mbona waliozidia ?
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Walikuwepo rijali, mbona waliozidia ?
Uovu hawakukubali, kwa kesho kuihofia,
Kahfu kawanakili, hikma alojaliwa,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Walifanza bilkuli, maovu kuyakimbia,
Mola kawapa akili, shimoni wakaingia,
Wakalala hai hali, karne ikatimia,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Dunia kuikabili, miaka inshapotea,
Watu walipowasaili, ukweli wakagundua,
Mola wakamkubali, na kutubu shirikia,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Mola tukimrudia, hayo yote hutuvua,
Subira tukiandaa, muda hautapotea,
Siku itajaingia, nakama tukazivua,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Ni wafu tuliokuwa, njiani tunatembea,
Maisha wamechafua, hakuna cha kujivunia,
Na motowakaribia, huku pepo wakimbia,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

NCHI naiombea, huruma sasa kupewa,
Balaa kuziondoa, na aibu ilokuwa,
Uhai tukaupewa, na uzima kuingia,
Kufilisika kubaya, lakini baya zaidi:
Uongozi muflisi !

Z a m a z a k e z i m e i s h a !



Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Sasa ni kushindanisha, washindani watakiwa,
Na kataa kupotoshwa, vyama vingi si ubaya,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Anza kujitayarisha, hakuna kubaguliwa,
Wao wakikuzamisha, wengine hukuibua,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Na wenzako kuamsha, wajibu unatakiwa,
Hivi sasa ni kukesha, kulala ni kukataa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Hakuna wa kuzungusha, chao mapema kutwaa,
Sasa utawagoganisha, timu nyingi kuchagua,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Na wanaokuchokesha, kila jambo kungojea,
Sasa kuwachangamsha, kugura kuwatishia,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Magamba walojivisha, hawawezi kuyavua,
Hata wakijitingisha, kutoka litakataa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Gwanda wanaojivalisha, anza kuwachungua,
Kama hawajabebeshwa, wanaweza kukufaa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Njaa iliyowachosha, pia kuwatembelea,
Huenda kitu kuzusha, wakakushangilia,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Kadi wakikukopesha, unaweza kuingia,
Mkakati kuanzisha, nchi ukapigania,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Yamejaa mageresha, inafaa kuwatoa,
Mimi wakinichongesha, ufunguo nitakuwa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Wamejaa washawasha, hofu mwilini kuvaa,
Kidonda hukutonesha, ukabakia walia,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Wako pia mabahasha, wa mabara na visiwa,
Madudu ukianzisha, huweza kufanikiwa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Kuna kina jumlisha, na wengine wa kutoa,
Hesabu ukianzisha, wengi budi kusinzia,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Ni kutafuta maisha, mradi umeingia,
Dira, dari imezusha, nani anaona njia ?
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Vijijini kuamsha, ukweli wakaujua,
Yavia yao maisha, kimoja kushikilia,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Na mikoa kuivusha, wingi huu watakiwa,
Serikali kuanzisha, za mikoa kutufaa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Kimoja hakikatosha, kuitawala mikoa,
Madaraka kugawisha, lazima itatokea,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Waliopo wachemsha, hakuna asiyejua,
Kazi watu wafundisha, kazini wameshakaa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Zama zake zimeisha, zama za chama kimoya !
Mengi sana yachekesha, na ukweli twaujua,
Mradi huu maisha, uongo vingine huwa,
Usikae katikati, sema uko chama gani !

Vua gamba, vaa gwanda


VAA gwanda, vua gamba, kijana wa Tanzania,
Hamnao uchumba, na hawa wetu mabwana,
Kiuchumi ni wagumba, yetu katu hayatafana,
Vua gamba, vaa gwanda,  amka Mtanzania !

Wamezoea kukumba, sio watu waungwana,
Chokoraa waso kamba, wenyewe twaumizana,
Ngonjera kazi kuimba, wafanyacho sijaona,
Vua gamba, vaa gwanda, mpate vinara wapya?

Kijijini kuingia, utajiri kuibua,
Kwa kilimo kutumia, mbadala nayo pia,
Dunia ikatujua, na ukweli uliokuwa,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Viongozi twaishiwa, mafukara hatujawa,
Nchi wanaichezea, na muda unapotea,
Sasa tumejichokea, tunataka kuwatoa,
Vua gamba, vaa gwanda,  amka Mtanzania !

Vijna wataingia, bungeni wasiosinzia,
Tundu Lissu mithilia, Myika na Zitto pia,
Nchi haitotambaa, itaanza kutembea,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Ajuza, shaibu pia, wamekwishajichokea,
Kustaafu kwawadia, wanapaswa kuamua,
Twataka damu mpya, kuifaa Tanzania,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Kabla ya kufikia, uchaguzi yatakiwa,
Wananchi kutumikia, kazi wakashuhudia,
Na sio kuugombea, ukubwa wa kujitia,
Vua gamba, vaa gwanda,  amka Mtanzania !

Mitaani kuingia, kampuni mkazua,
Kwanini twachelewa, mbona za umma mwazaa,
Na wananchi nao pia, kuwa nazo watakiwa,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Akili kuzitumia, na ofisi kukimbia,
Wananchi nao kukaa, yao kuzungumzia,
Kila kitu kina dawa, mengine mwatutania,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Vijiji budi kukua, ya msingi kupatiwa,
Na bomba zikachanua, kila mahali kutiwa,
Wamechoka kuonewa, maisha kusumbuliwa,
Vua gamba, vaa gwanda,  amka Mtanzania !

Na umeme nao pia, kila nyumba kuingia,
Benki kuu kudaiwa, huduma kuzilipia,
Hadi nchi nzima ikawa, iko chini ya taa,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Wao walituambia, nyasi watatulishia,
Ili rahisi kupawa, ndege ya kusafiria,
Sisi tunawaambia, ni vingine itakuwa,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!

Sisi tunawaambia, mishahara twakataa,
Hadi njaa kuondoa, hapa kwetu Tanzania,
Waso tayari inafaa, waanze kutukimbia,
Vua gamba, vaa gwanda,  msidanganywe vijana!


Mtoto sina lugha yangu

Mtoto sina lugha yangu

Baba, pia mama yangu, lugha hawajaniachia,
Ni yatima wa wazungu, makombo nategemea,
Na kigumu kichwa changu, vya wengine kusikia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Sijawahi mwona Mzungu, kuja kututembelea,
Nikifinyanga vyungu, ni wapi atanitokea ?
Na nikipata uchungu, yeye yangu atajua  ?
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Kama yangu ya uvungu, ninaweza kumwambia ?
Ulimi natia pingu, yangu lini kutambua,
Mswahili na majungu, mzungu na yake dunia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Alichotugea Mungu, hivi tunakitezea,
Sijui mdudu chungu, bila ya kusaidiwa,
Wazoza ulimi wangu, chetu sina nianachojua,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Kadhalika na wenzangu, hawaijui mimea,
Limeisha letu fungu, hatuna cha kusomea,
Nchi naiona chungu, mambo yake kufifia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Wanawajua Wazungu, wanyama tulojaliwa,
Huku kwetu ni mziungu, mwana gani awajua,
Ni chini ya yetu mbingu, lakini ibra wawa,
Ni yatima kwenye lug
ha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Vichwa tuumetiwa pingu, hatuwezi jitambua,
Hadhi yetu ya mabungu, elimu tunayopewa,
Cheo chetu sungusungu, wepesi kulaumiwa,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Kama tumelishwa kungu, kazi yetu kurembua,
Hata tupigwe marungu, vitu havitaingia,
Ila kama lugha yangu, nitaitesa dunia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Mbona nasoma Kizungu, na sio Kichina pia,
Wanacho nini Wazungu, wengine wasichokuwa,
Na mimi mahaba yangu, ni Mchina kwenda muoa?
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Kingereza na Uzungu,  mimi nini wanifaa,
Hali ninamcha Mungu, naelekea Arabia,
Na dini ni langu fungu, zaidi nitajisomea ?
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Ndugu na shangazi zangu, mbona wako Malyasia,
Nikisomea Kizungu, watasikia Korea ?
Na wazulu si wazungu, mbona chao sijajua ?
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Moyo wetu, moyo wangu, mwatutesa Tanzania,
Lugha hiyo siyo yangu, kwanini mwang'ang'ania,
Mwatukausha mawengu, si watu wa kutulia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Uturuki zama zangu, hata zenu mnajua,
Ni chao bila ukungu, na sasa wameshapaa,
Mkijitia uzungu, nini mwatusaidia ?
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Mafupi maisha yangu, ni kazi kujikomboa,
Muda huu sio wangu, mwazidi kuuchezea,
Hayaniishi machungu, kwa kushindwa endelea,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Kiswahili lugha yangu, ninaweza kutumia,
Zi wazi akili zangu, mengi sana yangeingia,
Iote mizizi yangu, mengine nikasomea,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Yakini wazazi wangu, digrii wangejipatia,
Kiswahili si uzungu, vyuoni vingetumiwa,
Na leo hii nchi yangu, hapa chini 'singekuwa,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Wamewanunua Wazungu, viongozi naambiwa,
Wataka sana kizungu, uchumi kutuibia,
Tuwe kama nyungunyungu, mvua kuitegemea,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Aliyebakia ni Mungu, shida yetu kuijua,
Na wale wenye uchungu, lugha kuipigania,
Elimu iwe ni mbingu, tu ndiyo yatuzuia,
Ni yatima kwenye lugha, mwana sina lugha yangu:
Za wengine natumia,
Sikuzote kufulia!

Hizi hapa bomba mbili


Bomba moja itaweza, kazi zake bomba mbili ?
Au ni kujishikiza, kungoja kitu kamili,
Kazi iweze kufanza, kwa haki na uhalali,
Hizi hapa bomba mbili, bomba moja itaweza ?

Kiasi chake hukuza, kwa idadi mara mbili,
Na kasi itafyonza, maradufu kulhali,
Na nguvuze za kuzoza, zinazidi mbavu mbili,
Hizi hapa bomba mbili, bomba moja itaweza ?

Wingi wake mwanagenza, ni kama pacha wawili,
Na mapipa huyajaza, yakazidi mara mbili,
Kuyabeba hutoweza, ila uwe na musuli,
Hizi hapa bomba mbili, bomba moja itaweza ?

Na pengine huchagiza, subira kama muhali,
Katikati kutokeza, pasiwe na afadhali,
Mkiacha yapooza, ni hasara mara mbili,
Hizi hapa bomba mbili, bomba moja itaweza ?

Kauli naikatiza, kwa maneno ni bahili,
Maudhui nimejuza, yanatosha bilkuli,
Mengina mtaagiza, tumieni 'imeili',
Hizi hapa bomba mbili, bomba moja itaweza ?

Utitiri haumwui




Hata kero hawawai, kwake mlalia mayai,
Katu hawajisumbui, wala hawawafikirii,
Na mchana hujiwahi, kwa vumbi kujistahi,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Ila sumu hiafai, wewe utakuwa mwui,
Dawa wangu simwagii, hili huwa ni jinai,
Nikazusha madai, kuupoeza uhai,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Utitiri hustahi, wakaangua mayai,
Vifaranga wako hai, nje wameshajiwahi,
Maji moto huzirai, utitiri ukiwahi,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Tena hapo hawakai, wameshaona nishai,
Huruka wakizirai, kwenda yao matlai,
Makazi kutanabahi, kuwa tena hayafai,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Kuku mama humuwahi, kwa dawa kumstahi,
Nao vifaranga hai, nyingi siwapulizii,
Hucheza wakafurahi, kero hawajionei,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Na jengine sinuni, yatosha kwao uhai,
Usafi siuachii, na maji kwa makarai,
Vinginevyo hawakui, kwa chema kujistahi,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Na majira yakiswihi, madhila hayarejei,
Nafuu ya jitimai, huwa tena haikawii,
Na shari haziingii, viumbe wasifurahi,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Matunzo hawakinai, viumbe madhali hai,
Na waja siwatanii, thawabu hutanabahi,
Ila wengi hawajui, wanyama  hawaridhii,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Tamati ninaitii, zaidi siongezei,
Ukarimu wanidai, wingi tena haufai,
 Nimekidhi maudhui, nyie zitoeni rai,
Kuku mlalia mayai, utitiri haumwui !

Saturday, May 5, 2012

Kiswahili ni mzizi


Nimeyaona Asia, Ulaya ni mazoea,
Lugha wanajivunia, hata kidogo wakiwa,
Nyengine kutotumia, ila nje wanapokuwa,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Chao wanajivunia, bila ya kusimamiwa,
Na kisha waongezea, vya wengine kuvijua,
Ubingwa kujipatia, kwayo na yale ya dunia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Asili waangalia, urithi kutopotea,
Pia rahisi ikawa, watoto kujifunzia,
Lughani wakichipua, mengi sana huyajua,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Leo hapa Tanzania, maneno yanapotea,
Ndege wetu kuwajua, wazima utawaumbua,
Sembese watoto kuwa, hawana wanalojua,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Wanyama nao pia, wawili watatu wajua,
Samaki waliojaa, bahari nayo maziwa,
Wangapi watakwambia, majina waliyopewa?
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Miti na mingi mimea, hakuna anayejua,
Utacheka nakwambia, mjini ukiulizia,
Afadhali inakuwa, kijijini wanajua,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Maumbo yake dunia, wengi utata hukuwa,
Bure utajisumbua, hakuna anayejua,
Na hawa wategemea, kitu kuja kuvumbua?
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Mizizi yake mmea, asili hutegemea,
Ndipo inapokuwa, kwa yote yanayokuwa,
Elimu ikiwa pia, muhimu kuzingatiwa,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Watafeli nadharia, kwa lugha kutoijua,
Watoto kuwakandia, ya uongo yalokuwa,
Walimu kuwazulia, hata wasiyofikiria,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Kiswahili kutumia, kufundisha nadharia,
Kwa undani kuelewa, yote yanayozungumziwa,
Haya wakishayajua, Kama China tutakuwa,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Tuitenge nadharia, na lugha kufundishia,
Maabara kufungua, shuleni na vyuo pia,
Lugha kuzikazania, mbili tatu wakajua,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Ndege wengi tutaua,kwa jiwe moja kutumia,
Sayansi wakaijua, na lugha kuzing'amua,
Hata Kiarabu pia, na Kichina kutumia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Mashariki inafaa, tuanze kuangalia,
Isiwe tunachelewa,
Wenzeetu wakatangulia,
Lugha yetu kujitia, lakini kutokutufaa,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Viongozi watakiwa, uzito kuuchukua,
Wafanze kuyaamua, mapema inavyokuwa,
Nami sintoshangaa, wengine kutangulia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Kiingereza balaa, ujanja wanatumia,
Lugha yetu kuiua, na yao kuendlea,
 Na sisi kamamajuha, mtegoni twaingia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Nyerere alianzia, lugha kasaliti pia,
Mwinyi alipofatia, naye akazainiwa,
Mkapa hakujitambua, wala hatajitambua,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Kikwete asipojua, humo humo kufatia,
Kiswahili kukiua, na elimu nayo pia,
Ndicho kilichobakia, na ndiyo yanayotokea,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Ila mtunzi najua, rais wa Tanzania,
Kweli atakayekuwa, Kiswahili ataamua,
Kila ngazi kutumia, na nchi ikaendelea,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Kwenye kapu watupiwa, wote waliotangulia,
Takataka watakuwa, kati yetu historia,
Nafasi waliipewa, ila hawakuitumia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Yajifia Tanzania,
Na pengine kung'olewa
Utamaduni huvia
Taifa lije lemaa
Asili ikapotea
Uvumbuzi nao pia
Watu wabakie kuwa
Vya wengine watumia
Pasiwe kitu kimoya
Wao wanachogundua!


Kuthubutu hapakua, na kujaribu wapwaya,
Hakuna walilojaliwa, kuliweza na kujua,
Waigaji wabakia, ni wasanii bandia,
Kiswahili ni mzizi, ukikatwa mti hufa:
Twaizika Tanzania,
Hali hai yapumua
Kwa kutokujitambua
Na kesho yetu kujua
Wakubwa wanunuliwa,
Cha watu kung'ang'ania
Wengine wajihadaa
Dawa ngeni wakidhania
Kumbe muda wapotea,
Milele nyuma kubakia,
Hamsini yaishia,
Itapita pia mia,
Hapahapa twabakia !


TTRKPP LIMITED 2012

Lugha ngeni watumia



Lugha yetu yachukiwa, tena yadharauliwa,
Wapambe wlaliokuwa, nchi tumewaachia,
Kushoto waelekea, sisi twataka kulia,
Lugha ngeni watumia, wabakia ujingani !

Yabadilika dunia, jueni Watanzania,
Mzungu anafulia, kila mtu anajua,
Bado twawafuatilia, nasema tunapotea,
Sasa wanaajiriwa, makoloni yalokuwa,
Lugha ngeni watumia, uzungumze na nani ?

Sisi bado twasinzia, maajabu twategemea,
Naona huu udhia, siwezi kuvumilia,
Kweli ninasiimulia, haraka tujue waa,
Lugha ngeni watumia, unafeli mitihani ?

Kila kitu huzaliwa, na kufa  ni yetu njia,
Hata lugha nazo pia, wakati hujafikia,
Kihali zikaugua, na kufa ikafikia,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kichina ?

Twatakiwa kuchanua, lugha nyingi kuzijua,
Maabara nawambia, za lugha zinatakiwa,
Huwezi jisomea, darasa halitofaa,
Lugha ngeni watumia, basi iwe Kifaransa !

Darasa sio radhia, maabara yatakiwa,
Sayansi hutumiwa, lugha nyingi ukajua,
Kusoma na kuongea, rahisi sana ikawa,
Lugha ngeni watumia, kwanini si Kiarabu ?

Bora teknolojia, hivi sasa zatumiwa,
Na katika wiki kadhaa, mtu lugha huijua,
Msada ukabakia, kila siku kujitia,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kihindi ?

Maabara hutumiwa, kwa lugha tu kusomea,
Madarasa kubakia, lugha mama kutumia,
KIzazi kikajijua, na urithi kutopotea,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kireno ?

Haya yanayotokea, wakubwa wanapotea,
Kasumba imewajaa, wamekuwa historia,
Yabadilika dunia, wao nyuma warejea,
Lugha ngeni watumia, wabakia ujingani !

Kilio ninacholia, mwatakiwa kuchukua,
Ujumbe ukaenea, na chetu kupigania,
Tusiachie oraa, ndio wawe mashujaa,
Lugha ngeni watumia, uzungumze na nani ?

Mkienda Malaysia, lugha yao watumia,
kadhalika Indonesia, lugha mama inang'aa,
Aidha nako Korea, si n yingine watumia,
Lugha ngeni watumia, unafeli mitihani ?

Na elimi imejaa, mizizi ilojaliwa,
Si ya ghibu kutia, bali kichwani yakaa,
Uvumbuzi waumua, kila ktu wagundua,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kichina ?

Tumechagua kuua, lugha yetu asilia,
Hakika sisi majuha, najutia kuzaliwa,
Uwezo ningelikuwa, hili ningelikataa,
Lugha ngeni watumia, basi iwe Kifaransa !

Bahati twaichezea, shilingi tuliyopewa,
Chooni twaichezea, yaja sasa tumbukia,
Na ikisha tumbukia, tuone kitakachotokea,
Lugha ngeni watumia, kwanini si Kiarabu ?

Msishindwa wazamia, wapenzi msiokuwa,
Watu wawanyapaa, kwa chenu kukitetea,
Wala si kuwachukia, bali huruma kujaa,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kihindi ?

Huruma kuwaonea, inafaa Tanzania,
Wameshindwa jitambua, waenda kusikofaa,
Bila idhini Jalia, utumwani twarejea,
Lugha ngeni watumia, kwanini sio Kireno ?

Dawa dua na kufunga



MOLA tukimgeukia, huwa yasiyowaziwa,
Na wanaojipangia, yao yakapanguliwa,
Inahuu yakidunaa, waakidu kaydaa,
Dawa dua na kufunga, viongozi mafisadi !

Mbali ninaangalia, hakuna lilo sawia,
Arijojo nahofia, ndio tunakoelekea,
Upepo umepungua,  nguvu wajikusanyia,
Dawa dua na kufunga, wabunge wanaohonga !

Kiumbe hatoitoa, nusura ninayoijua,
Uwezo wameishiwa, si watu wa kujaliwa,
Toba wameikataa, nia zao kutimia,
Dawa dua na kufunga, mahakimu wadhalimu !

Shiriki wanakazia, njoo jua, toka jua,
Tambiko kuabudia, nazo taslima pia,
Wengi wameshapotea, nasi tunajionea,
Dawa dua na kufunga, wanasiasa waovu !

Dini wazikatalia, ibada kuzingatia,
Shere wakawafanyia, wanaowaaminia,
Wajinga wakadhania, rahisi kuwahadaa,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

Nafusi zawahadaa, katika hii dunia,
Bora wanajidhania, viumbe wa kuzaliwa,
Mifupa wajaokuwa, muongo haujaishia,
Dawa dua na kufunga, viongozi mafisadi !

Dhamana waitibua, na uongo kutumia,
Heri wanaikataa, moto kujipalilia,
Siku zinahesabiwa, na wao hawajajua,
Dawa dua na kufunga, wabunge wanaohonga !

Waja ninawaambia, ni kufunga nazo dua,
Ndio sasa zatakiwa, maamuzi kuamua,
Aachiwe wa kuachiwa, kitu asiyekosea,
Dawa dua na kufunga, mahakimu wadhalimu !

Naapa tukimrudia, tena hatutapotea,
Tawba ataitoa, na nuru kutujalia,
Iwe njia twaijua, si wao kufuatia,
Dawa dua na kufunga, wanasiasa waovu !

Na wanaonunuliwa, hao wameishapotea,
Duania waidhania,  ndio bora ilokuwa,
Kumbe mkenge waingia, kwani hawajajitambua,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

Ninamaliza kwa dua, kumwangukia Jalia,
Na sujuda kuitia, chini nikanyenyekea,
Hatuna pakukimbilia, ila kwake kurejea,
Dawa dua na maovu, kwa vyama vinavyoiba !

Ubunge kujitolea



WAKATI umefikia, tume ninaiambia,
Kwa posho tu kuitoa, mishahara kukataa,
Mbunge akapatiwa, kaziye kujifanzia,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Ubunge wakimbilia, hata wasiotufaa,
Kisa kwenda kujilia, uhondo uliojaa,
Hili budi kuondoa, ikawa kujitolea,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Sasa wa kuulilia, hatokuwa mwenye njaa,
Mbali ataukimbia, mengine kujifanyia,
Wachache wakabakia, sisi wanaotufaa,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Kingereza wasojua, hapa hawatoingia,
Elimu itatakiwa, na ujuzi kujaliwa,
Na kisha mtu kupewa, kiwango alichokuwa,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Siasa zatuchafua, ujira mkubwa kutwaa,
Kiwango wasichofikia, wala kuwa na manufaa,
Hili sintoliridhia, kuliwa na wasojua,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Ajira nayo wakiwa, bora zaidi 'tkauwa,
Kampuni zao kuwa, ndizo zinazowafaa,
Na bungeni kuingia, iwe ni yao ridhaa,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Tundu Lissu wengi kua, bungeni waliojaa,
Sio wanaosinzia, pashioni kujilia,
Pembeni hao watakaa, na hawatovumiliwa,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Daktari watakiwa, kulipwa kilichojaa,
Maisha waokoa, sio hao kusinzia,
Nchi itaendelea, tukiishi kwa afya,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Walimu wanatakiwa, maslahi kupatiwa,
Sio wanaoongea, kitu wasichokijua,
Haya tukishapindua, ubabaishaji huvia,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

Bunge busara kujaa, na watu waliotulia,
Hekina wakatumia, wote wanoaingia,
Sana kuzungumzia, ya nchi yetu kufaa,
Wabunge wajitolee, kulipwa ni ufisadi!

IBILISI KANAMBIA


Ahadi nimepokea, Lucifer keshanifaa,
Urais kuujua, nikaongoza dunia,
Na ukubwa kuutwaa, wateteme wenye njaa,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Nitabagua kwa nia,  kundini mwangu kujaa,
Kila mwenye kunifaa, ndio wa kumchagua,
Nao nisiowajua,  litakuwa bati baya,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Warembo nitachagua, Ikulu kuifagia,
Aidha kunipikia, na miguu kuangalia,
Masaji na kunichua, hayo sintoulizia,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Wahuni nitachagua, ulinzi kunifanzia,
Iwe panga ni pangua, hawi nami asokuwa,
Salama ni kukimbia, salama kisichokuwa,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Wazawa nitabagua, mali kujabarikiwa,
Ila wageni wafaa, rushwa nyingi wanatoa,
Hawa nitawaangalia, hata kama budi kuua,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Anasa nitachagua, aghali zilizokuwa,
Na vyombo kuvinunua, urahisi kuutia,
Na kitakapopungua, hatia mtu namtia,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Na nguo sintozivaa, tena nikzirudia,
Viatu nitavitia, kila aina vikajaa,
Marashi nitajitia, bei mbaya yalokuwa,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Sultani nitakuwa, hakuna wa kukataa,
Katiba nitabomoa, ya kwangu kujiundia,
Mlango ukifunguliwa, ukifufunga mzaha,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Dunia nitatembelea, hata kipofu nikiwa,
Mengi nitajionea, sina nitalochukua,
Umaskini yetu ndoa, misaada kujipatia,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Msije kunizulia, hata nisiyoyajua,
Ninaganga yangu njaa, raia wajitegemea,
Mkate wasipopewa, keki nitawagawia,
Ibilisi kanambia, urais atanipa !

Neno toka mafichoni



WAJE juu na madege, na helikopta pia,
Wapambe kama nzige, anga na hii dunia,
Naweza nisiwaige, bado nikawanyanyua,
Neno toka mafichoni, linaweza kuwa dawa?

Hakika mfanywa bwege, neno lake akijua,
Yumkini wamroge, ndio chini  hutulia,
Ujinga tena afuge, kwake huwa ni nazaa,
Neno toka mafichoni, maskini kaamini?

Keshalikinai bunge, yake haliwezi jua,
Na japo mchafukoge, kuringa yake ridhaa,
Mpeni maji aoge, yake mkayaachia,
Neno toka mafichoni, mayatima waridhia ?

Watu hawajawa ndege,tunduni mkawatia,
Maishani muwafuge, uhuru kutowaachia,
Huja waje walichonge, sawia lililokuwa,
Neno toka mafichoni, wasonacho walijua ?

Haijengwi kwa mizengwe, hii yetu Tanzania,
Haya bure mjivunge, mtakuja sanzuliwa,
Na wenyewe mjiroge, wengine kusingizia,
Neno toka mafichoni, linaweza kuwa dawa?

Demokrasia kikongwe, kila kitu inajua,
Elimu budi mlenge, msojua kurudia,
Burebure msijikoge, kaburi mwajichimbia,
Neno toka mafichoni, maskini kaamini?

Yapo yasiyo matege, twaweza zungumzia,
Na chama chenu mjenge,mambo mkafanikiwa,
Vingenevyo mringe,nasi tutawaangalia,
Neno toka mafichoni, mayatima waridhia ?

Twataka nchi mjenge,ushabiki twakataa,
Wabora wenu muige, uongo kutokuzua,
Nyoyo za watu mkonge, ridhaa mkapatiwa,
Neno toka mafichoni, linaweza kuwa dawa?

Ubabe budi mbwage, au utawaambua,
Watu ovyo msipige, madhambi mkayavaa,
Laana muwe vihongwe, mkaja kuachiwa,
Neno toka mafichoni, maskini kaamini?

Kirini ulegelege, ndani umeingia,
Gamba ili 'litokage', nusunusu kutoachia,
Na mkitaka 'mlindwagwe', wapo wa kushikilia,
Neno toka mafichoni, mayatima waridhia ?

Kengele sasa mpige, upya mpate zaliwa,
Ajizi msikoroge, sumu mkajinywea,
Ukweli msijivunge, vijan wawakataa,
Neno toka mafichoni, wasonacho walijua ?

Kisa wao mwatenge, kuzaa na wa kutozaa,
Mkayaweka magenge, utu kujivurugia,
Kisha wenu muwafuge, wengine kuwaachia,
Neno toka mafichoni, wasonacho walijua ?

Waona kanga na vitenge, mjini mkivigawa,
Vijijini muwakoge, uongo kuwaachia,
Na mbele wasisonge, karne yakaribia,
Neno toka mafichoni, wasonacho walijua ?

Haukunipa sadaka


Haukunipa sadaka, niliponyoosha mikono,
Ulionyesha mashaka, nikasikia mguno,
Na nyuma hukugeuka, macho yaje makutano,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Yangu yangelikufika, usingedhani kivuno,
Huku nilikovunjika, ni pamoja na kiuno,
Ni wapi pakusimika, ila hapa makutano,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Mjinga sijaerevuka, akili zangu ni ngano,
Zamani nilisikika, hivi leo ni agano,
Mtu asiyehitajika, hivi ana mabishano?
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Kwenda kwangu kwa hakika, na wala si mapishano,
Rahisi lingejengeka, kbala mfarakano,
Nimeacha ya kuzuka, yatakuwa mshikamano?
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Nakuomba sikutaka,  bila ya mivutano,
Ahadi yangu si shirika, usio ushirikiano,
Hapa nimepumzika, natazama wenye neno,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Hali yangu ya kizuka, inangoja mazikano,
Daraja siwezi ruka, hapo sina  mlingano,
Kichwa kitanipasuka, kwa huo msuguano,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Ndio mwisho ninafika, hapanalo tangamano,
Imekwisha Tanganyika, Tanzania sio neno,
Wameisha Waafrika, imebaki michuano,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Yako sana nilitaka, kufuatia kisigino,
Nilidhani malaika, ningelkuwa na maono,
Hadi nikaweweseka, nilipotia tabano,
Nilinyoosha mikono, haukunipa sadaka !

Mwafrika mnafiki


Kiumbe haaminiki, wala hatelekezeki,
Hadhira isimlaki, bila ya kumhakiki,
Ni kubwa yake ashiki, ukwasi kuumiliki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Lini ikawa riziki, kiumbe anayemiliki,
Historia yashtaki, Maghairbi, Mashariki,
Kiumbe kutamalaki, kuizidisha hamaki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Ni kiumbe mabruki, lakini hafadhiliki,
Haliye huishtaki, hata kwao mushriki,
Na kwingine habebeki, uwezo hutaharuki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Anampenda Mali, awe mkubwa rafiki,
Ila yeye adhihaki, ucha mungu hautaki,
Na Mola hababaiki, kama yeye habebeki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Ni milki na milki, wamejaa wanafiki,
Na wasio taharuki, huwafukia handaki,
Wakawa hawazoleki, hadi Barru kuafiki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Nami hili siafiki, daima nawashtaki,
Hata kama sipendeki, sintokuwa mamluki,
Ni heri nikafariki, kwenda mbali kushtaki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Njia zangu za Sadiki, wala sio unafiki,
Mungu wengi sishiriki, hayo hayavumiliki,
Tawhidi namiliki, udhibiti nahakiki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Yake hayatabiriki, mishtuko sidhihaki,
Nahofu haambiliki, isije kwangu riziki,
Nipate kilicho haki, uongo nisiafiki,
Mwafrika mnafiki, mwenyewe ajidhihaki !

Huwezi danganya kifo



Uzee ukiingia, kitu gani wangojea,
Vipi iwe ni hadaa, Jibrili kakujia,
Muda akakuachia, kuibadili tabia,
Watu utawahadaa, huwezi danganya kifo !

Muda akakuachia, kuibadili tabia,
Nawe unajihadaa, nguvu mpya kujitia,
Huna unalolijua, kiumbe unapotea,
Watu utawahadaa, huwezi danganya kifo !

Nchi utaiachia, wengine kuendelea,
Yako yakajaishia, kumbukumbu kubakia,
Ubaya ukizidia, zaidi kukumbukiwa,
Watu utawahadaa, huwezi danganya kifo !

Afrika inalia, uongozi kutokua,
Arijojo waelea, hawajui pakutua,
Mibabe tumeachia, damu tuanjimwagia,
Watu utawahadaa, huwezi danganya kifo !

Nusura hatutajua, bila Mola kumlilia,
Kisha kumshtakia, viongozi kutokuwa,
Yeye akatuandalia, bora watakaotufaa,
Watu utawahadaa, huwezi danganya kifo !

Wanafiki mtaona



Mnafiki hufurahia, mwenzie akiumia,
Moyoni huzawadiwa, roho mbaya kujaliwa,
Kufa ukatarajia, yeye hakuandikiwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Mapema walitakiwa, salama kuzingatia,
Wao wakayaachia, hadi kwingia pabaya,
Kama mamba watatoa, machozi maji yalojaa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Taifa wanaligawa, kwa wanayokusudia,
Njia hawajaijua, wameanza kutembea,
Mashimoni kuingia, nani atawashangaa?
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Porini wataingia, msitu hawajaujua,
Swala anapotokea, duma watamdhaia,
Na wakianza kukimbia, mbio hawatamfikia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Moshi wanaukimbia, kumbe motoni waingia,
Macho hawakufungua, nini utatarajia,
Kazi yao kuambiwa, wakabaki itikia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Madhambini wawatia, hata sffi walokuwa,
Uongo wakaujua, kwalo wakabarikiwa,
Kama si kulaaniwa, kama ninavyoelewa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Kuiba waumbuliwa, ujanja wapakuliwa,
Chungu kinachobakia, halali kimebakia,
Imetamka dunia, mwisho unakaribia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Maneno kuitikiwa, zamani ilikuwa,
Sasa vitu vyatakiwa, machoni tukavitia,
Midomo mngeshonea, kwa sindano na shazia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wazo likishazaliwa, ni vigumu kuliua,
Mwaweza watu kuua, ila wazo labakia,
Na kila ukizuia, ndivyo linavyochanua,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wakati ukifikia, liwalo lazima kuwa,
Hakuna wa kuzuia, hatangani angekuwa,
Jaribu utaumia, ukabakia kulia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Ukuta ninawaambia, ndivyo wakati huzua,
Na usiyotarajia, konkreti huja kuwa,
Na ngumi ukiitia, kuvunjika waridhia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Nchi inatakiwa, ushindani kuulea,
Wachungu wawili kuwa, au zaidi yafaa,
Na nyote kupigania, ya haki yaliyokuwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Ukitaka ng'ang'ania, utamu kuukamia,
Rahisi haitokuwa, uchungu kuukataa,
Hakuna aliyezaliwa, kutawala kajaliwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Nusu kura wakataa, hamuoni ni udhia,
Sababu hamjajua, na gamba hamjavua,
Uoza mnatumiwa, na hayo ndiyo maua,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wakati umewadia, fakiri kuangalia,
Nao pia ni wazawa, na fursa walilia,
Wenyewe kujichagua, pabaya mtaingia,   
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wagonjwa twawaombea, Mola kuwaangalia,
Maumivu kupungua, na nafuu kuijua,
Afu tunakulilia, na haki kuangalia,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!

Wa kawaida raia, hospitali watakiwa,
Kuwaonyesha wakiwa,  upendo uliojaa,
Wakubwa wakikataa, bora zaidi itakuwa,
Wamafiki mtaona, wagonjwa watembelea!


Ya Saudi Arabia



Usiwe nayo hasira, ya Saudi Arabia,
Watakiwao subira, kushindwa kuvumilia,
Uwe kama vile fira, jinyoka lenye kuua,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Na uongozi imara, hili jambo watambua,
Hawaitaki papara, za wenyewe kuumia,
Ramani huwa wachora, huku chini watulia,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Hakuna aliye bora, kiumbe wa kuzaliwa,
Mwaipandisha Hasira, ya Muntaqimu Jalia,
Hatowapa maghufira, juu mkijinyanyua,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Hii ni yangu bishara, mtawala kumwitia,
Aiepuke hasara, Ahadi kukusudia,
Na atoe manusura, mfungwa kumuachia,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Ninayaona madhara, kwa  ndugu kujiumbua,
Hayo yote si tijara, ni chuki yanayolea,
Na mkizikosa fikra, wote mtajapotea,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Dini yetu ni stara, magomvi kutozua,
Hasa kwetu walo bora, na ndugu tuliokuwa,
Wazandiki watuchora, hili wanashangilia,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Yabadilika majira, udugu kuukazia,
Dunia ni masihara, Islamu waumia,
Mkiitia mikwara, machungu yatasambaa,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Tunataka uimara, na wala sio kupwaya,
Si nyoka vipi mwafura, au shetani mwamwachia?
Twawaombeni hadhira, tatizo kulitatua,
Au sumu utatia, pale isipotakiwa !

Huu ni wakati wetu



TWAPASHA wazazi wetu, miaka yao yaisha,
Walikuwa ni wenzetu, sasa wanajipaisha,
Ama nao kati yetu, ududu umeshakwisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Hii sasa mida yetu, ni nani anayebisha,
Viti vyenu, viti vyetu, twawaomba harakisha,
Na wanenu si wenetu, nasi twaanza zalisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Tuliwakopesha utu, mwatulipa magarasha,
Mwatugeuza viatu, tena vilivyokwishaisha,
Kumbe watu wana kutu, hilo latufadhaisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Mmeifyeka misitu, mkimaliza maisha,
Na kwa wenu ubutu, mwateta mwala maisha,
Sisi sio watukutu, ila kweli mwatuchosha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Mlitutia ufyatu, kwa dola kuritadisha,
Ibilisi kawa mtu, ndani mwamkaribisha ?
Hakika sio wenzetu, mmekwishatuonesha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Mtatutia vigutu, pindi tusipowakomesha,
Mioyo yenu kama chatu, ndio maana twaisha,
Kweu mchafu utatu, mliokwishauanzisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Wakowapi kina Tutu, chini wakawaketisha,
Wetu wana ukurutu, wanangoja kushibishwa,
Naona hamna kitu, wesha kabla ya kwisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Hawa wetu ni Mobutu, wangoja siku kuisha,
Wengine heri vifutu, waweza jislamisha,
Sio Moro si Kidatu, hawana cha kuzalisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Daladala ni matatu, jina wanabadilisha,
Mtu hawi ni kiatu, guuni ukajivisha,
Ndio hayao mwanakwetu, ama kwetu si maisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Lao haliwi ni letu, ila watufananisha,
Nisisngecheza upatu, msingi wangeanzisha,
Kwangu si heri mtutu, zogo sitaki anzisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Na makwao sio petu, vipi wajeniwezesha,
Nyumba iwe sio kitu, ila mali kuzalisha,
Hao nao sio watu, hili wangeshaanzisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Wametugeuza ratu, sangari kuikomesha,
Hakika maji matitu, jihadi wanaanzisha,
Binadamu bila utu, huwezi ukamtisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Na utu hauwi vitu, hili nawaelimisha,
Wito wenu sio wetu, haya tusipopitisha,
Sasa ni maisha yetu, ya kwenu yameshaisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Sasa ni maisha yetu, ya kwenu yameshaisha,
Acheni nafasi zetu, hali kuziimarisha,
Mkatoa tahyatu, sala mkahitimisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !

Malindi hadi Tumbatu, Shinyanga hadi Arusha,
Kwenye dhahabu na msitu, nia tunawakilisha,
Kiilichokuwa ni chetu, lazima kututajirisha,
Huu ni wakati wetu, zama zenu zimekwisha !