Saturday, June 12, 2010

Uongozi kama kazi

Haujesha usingizi, mjue wenu watani,
Kazi gani uongozi,mradi kono kinywani,
Na hawajitoshelezi,vipi wawaangalieni?
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Wewe hawakuwazi, rohoni bali mdomoni,
Mwageuzwa vijakazi, kwenye kura wabebeni,
Wakishaipanda ngazi,milele hamuwaoni,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Wawatia bumbuwazi, kukejeli yenu imani,
Nanyi kama madowezi,ujanja hambaini,
Mwafikiria andazi,wenzenu wako angani,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Hatuwaiti wapuuzi, lakini mna walakini,
Funza mwana hamfunzi, kujipachika kidoleni,
Uweje ni bazazi, yako yakose thamani,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Maisha ni utelezi, mara hujikuta chini,
Na uliyempa ngazi,hutoa usiamini,
Ukakosa kiegemezi,shurti kukaa chini,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Tunachagua machizi, twawapa kushika mpini,
Majembe na vifyekezi, twavishika kwa chini,
Wakivuta hawawazi,kinachotokea ni nini?
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Uongozi kama kazi, hii ajira makini,
Waweza kupiga dozi,siku nzima ofisini,
Na kukosa hauwezi,mshahara hutumiwa,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Nawauliza wajuzi, jambo hili nambieni,
Jengoni wenye mizizi,na mitaa hawaioni,
Kweli hawa viongozi,au wasanii shani?
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Uongozi kama kazi, nani awaongozeni,
Watu wataka mabenzi,sio kuwaokoeni,
Nyie kama nguvu kazi,lazima wawatumieni,
Uongozi kama kazi, mkono wenda kinywani.

Ndoto njema

Usiku uliopita, ndoto njema niliota,
Jina lako niliita, kuitika hukusita,
Nilipo ulinifuata, napo tukaanza teta,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Kisha nilipokuvuta, ulikuwa kama uta,
Au nyuzi za gitaa, ukaja bila kubwata,
Shingoye ikafyata, uso wangu kuukuta,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Vidole niliviita, navyo vikanikumbata,
Mikono nikakamata, mwili wangu ukitweta,
Na midomo kuifuta, kwa vidole vikanata,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Jina lako nikaita, ukamwitika mwiita,
Pua yako nikakuta, na masikio kung'ata.
Kidevu nikakamata, na mashavu kuyakita,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Ndoto niliyoiota, surayo yameremeta,
Pumzi nilizozivuta, ujana nikaburuta,
Na mavune kuyasuta, nguvu mpya nikachota,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Kamba hii naivuta, sitaki kukukokota,
Njoo bila kusita, nyota njema inaita,
Wewe sio wa kupita, bali tujenge manyatta,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Nafaka nikizichota, fifi nitazipepeta,
Ungo nilioupata, kutumia sitosita,
Na kazi sintoiwata, ili na watu kuteta,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Ninawajuza wa Mvita, Kibarani na Taita,
Ninayataka makata, udi, uvumba mbatata,
Kunuiza vya kupata, kama asali na nta,
Ndoto niliyoiota,siamini, siamini!

Kukuru kakara

Mtu wa tambo na visa, asikutie mkwara,
Watu hawa ni asusa, raha yao ni kukera,
Na wengi kama si tasa, basi hawana madhara,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Na wengi kama si tasa, wa mawazo na fikra,
Hawajawa mamajusa, kutabiri lilo bora,
Changamoto na fursa, kwao hazina tijara,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Hawaasisi kabisa, kazi kufwata bendera,
Njiani wanapapasa, hata mwanga uking'ara.
Na macho ni kupepesa, hawaioni ishara,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Wanatamani anasa, kwa ufisadi na ukora,
Kazi ngumu huzisusa, utadhani machotara,
Si ndizi ni kibubusa. hawachi kuja fura,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Hakika ninawaasa, hii iwe yenu sera,
Wasiwatie mkasa, watu wenye masihara,
Fungeni vyenu vitasa, barazani watadorora,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Mtenzi sina darasa, ningeliwapa ibara,
Masimulizi na visa, vya haokukuru kakara,
Vibaya walipojitosa, na kujikuta akhera,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Wafupi hutaka disa, urefu huwezi pora,
Pua ni ya kunusa, vipi wataka ipura,
Aliyejaliwa utasa, dawa yake maughufira,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Huwezi toba kususa, kuna Ibura kama za Sara,
Ufakiri sio posa, ndoa huweza kugura,
Jaha ikishakugusa, huwezi pata hasara,
Kukuru kakara ada, kwa madebe yaso kitu.

Nikifa sherehekea

Halijawa majaliwa, lile lisilojaliwa,
Pindo sio sawasawa, wala mstari kuwa,
Kama nilivyozaliwa, ndivyo nitavyojifia,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Nikifa sherehekea, pengine utajaliwa,
Milele hapa kukaa, hadi siku ya ukiwa,
Ahadi sikujaliwa, mie ni mpita njia,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Siku ninaichukua, kila ikija hatua,
Sina la kulikamia, lijalo ninaridhia,
Ndivyo nilivyozaliwa, vinginevyo sijawa,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

4.
Hali yangu naridhia, sitaki kujishaua,
Nilicho nacho najua, ndicho ninachotumia,
Cha wengine sijajua, labda kipotee njia,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Edison atambua, haachi kunishangaa,
Nacho nilichokuwa, kidogo pia natoa,
Elimu na ya dunia, sijui kulimbikizia,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Sehemu kaibania, mashairi kupungua,
Aona namzulia, wa kutunga ni mmoya,
Sio raha ni karaha, sasa kwake nimekua,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Hawajui tangazia, cha ndani kilichokuwa,
Japo tumewaambia, wangali wanasinzia,
Wao jipya la kuzua, ukurasa kubania,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Na ndivyo walivyokuwa, binadamu nakwambia,
Wengi wa kukotoa, ila hawawezi toa,
Wengi wa kushangilia, ngoma wasioijua,
Nikifa sherehekea, ili uishi milele!

Waja kisha huondoka

Si wa kutumainia, Waja kisha huondoka,
Hao ni wapita njia, sio watu wa kukaa,
Wana lao wanajua,lako hawewezi shika,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Wanatalii dunia, uwezo wameushika,
Kila wakikuchekea, ni kicheko cha dhihaka,
Hawatakusaidia, hapo ulipo kunyanyuka,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Mbwata matako hulia, wakiapta cha kushika,
Sinema kwao dunia, hutazama wakacheka,
Na wao kufurahia, neema walizodaka,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Katu hautoingia, katika yao hakika,
Hesabu imetimia, wewe hawajakuweka,
Wewe ni wa kutumiwa, sio wa kutajirika,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Hawa ukishawajua, vizuri utajiweka,
Kaa huku watambua, wewe kwao ni wahaka,
Chombo kinachotumiwa, mali zikazalishika,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Wafaa hukusifia, na vilivyo kukupika,
Ili uwe manufaa,watakapo wakafika,
Na mengi hukuachia, ili wewe kuridhika,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Ila kaa ukitambua, kwa mtu kma kiraka,
Hubanduliwa tambaa, au nguo kuchanika,
Na hivyo ikishakuwa, hutupwa kwenye majaa,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Niongoze ya -Jalia, kwa changu nikanyanyuka,
Hapa nilipofikia, naomba zaidi kuvuka,
Inifae hii njia, kizazi changu kushika,
Waja kisha huondoka, sisi ni wapita njia.

Fukwe ni za wenye nacho

Masikini hana chake, fukwe sio tena yake,
Sasa fensi usivuke, pembe zote waeleke,
Kama mwana, mtu chake, asiye na fedha lwake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Pwani mshikemshike,wapi kwao kukalike,
Tokea watu wazuke, na wengine wazuzuke,
Mme hamjui mke, na dada hana kakake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Yabaki tumemetuke, wengine wangangaduke,
Kiunga chako ni chake, akiingia utoke,
Usingojee mateke, labda haki iamke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Toka haki ibweteke, na virongosi wafoke,
Dhuluma iheshimike, na mabavu yajengeke,
Sera sasa teketeke, na mjai yawa mvuke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Mnyonge na anyongeke, tajiri atajirike,
Na asiyeko muweke, aliyemo abweke,
Sautiye ikauke, na mwishowe mmzike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kwa vipi waabudike, viumbe wala matoke,
Iweje waheshimike, vibaka kamavibweke,
Na lini tuneemeke, hali mali zisanzuke?
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Na ardhi itoweke, mikononi itutoke,
Wapi mbavu tuziweke, ijapo tupumzike,
Wapi pakanyagike,mabalaa tuyavuke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Ni haki tukereheke, mnyonge hana mwenzake,
Ni wapi avumilike, apate kilicho chake,
Na lini asalimike, asetiri moyo wake,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Mnyonge kabaki peke, uchumi tena si wake,
Mwache mlozi acheke,dhiki ni nafuu kwake,
Wacha hasidi wawike, uovu unawirike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kindakindaki mdeke, wenye nchi muezeke,
Vigae visigawike, na bati lisibwatuke,
Mvi zingekuwa mbwike, tungetaka tuzeeke,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kijigijii msuke, twafumua mfutike,
Pekupeku msivuke, miiba isije wateke,
Mchanga sichanganyike, hapa sikwetu msinizike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Sokomoko msitake, virungu msidundike,
Eleka mwana ueleke, kizazi chenu sio chake,
Chekeni wajinga mcheke, mwacheni anufaike,
Fukwe ni za wenye nacho, masikini hana chake.

Kumi na nane yatimu

Katujalia Alimu,imedumu yetu ndoa,
Na yetu mastakimu, hili yashuhudia,
Sasa ni ndugu wa damu, kaka na dada tumekua,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Jambo hili ni adimu, maisha yalivyokua,
Subira haikirimu, pupa mbele zimekua,
Wengi wana uhasimu, badala ya ngugu kua,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Umezidi uharamu, halali imekimbia,
Ulimi sasa ni sumu, ndoa nyingi unaua,
Wivu pia kutuhumu, navyo vinachangia,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Namshukuru Adhimu, toka kuwa mtarajiwa,
Hadi nikahi rahimu, tisini na mbili kua,
Nimemshika mwadhamu, nayeye kanishikilia,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Na machungu na matamu, yote tuliyachangia,
Hatuna cha kulaumu, Mwenyezi katujalia,
Twamwomba wetu Karimu, mbele kutuangalia,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Valentine baragumu, siku iliyobarikiwa,
Mimi na wangu dawamu, ndoa yetu ilikuwa,
Kama wema Waislamu, mashehe wakasomea,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Twamsihi Mukadamu, ya kwetu kutuafikia,
Tuwe watu wa salamu, wengine kutotegemea,
Ya kheri kutukasimu, wengine kuwasaidia,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Twakuomba ya Rahimu, isafishe yetu njia,
Twepushe na Jahanamu, kwa shetani kutukimbia,
Tupe yako ya Karimu, yaliyojaa ulua,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Kizazi chetu kidumu, katika sahihi njia,
Dunia isiwadhulumu, na wao kuitumikia,
Na jina langu lidumu, miaka itayofatia,
Kumi na nane yatimu, miaka yetu ya ndoa!

Usijisumbue

Bure usijisumbue, huko sintoangalia,
Mwana usijishaue, kiwango hujafikia,
La leo usidhanie, kama la jana itakuwa,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Muda usijipotezee, utakalo halitakuwa,
Maisha usichezee, hili hukuandikiwa,
Bahati isikupotee, kwingine nenda kimbilia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Hili usikimbilie, mwana litakukimbia,
Hapa usishikilie, gharika itakuzoa,
Matumaini yasijae, bahari ikajapwelea,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Karibu usisogee, usije ukaungua,
Macho usiyaachie, mwishowe utakujalia,
Mwili usiukaribie, peke yako kubakia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Hili hakika silijue, mengine waweza jua,
Hili usilichukue, lazima utaachia,
Hili usilitegemee, halitakusaidia.
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Na pepo zinipepee, mie si mtu wa kukaa,
Popte usinitembelee, peke yako utabakia,
Moyo usiniachie, ukiwa utakuvamia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Fanza moyo utue, kwa kutoroka tamaa,
Vitani usiingie, na silaha zilochakaa,
Ujibari ukimbie, kilema wajitakia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Ili nisikuzuzue, nikabu ningelivaa,
Nahofu wasielewe, macho nje wanotoa,
Ngoja nijinyamazie, na uziwi kujitia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!

Niache niendelee, na wangu mwenzi kukaa,
Sakura na uchague, utapata maridhia,
Si wako kamwe mie,moyoni hutonitia,
Usijisumbue bure, huna utachoambulia!
Hili halina maneno, wahenga wameafiki,
Ya nini mabishano, na hiyo mikikimikiki,
Muungwana si maneno, bali vitendo lukuki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Wataka ufungamano, bila kweli wadhihaki,
Kujenga mshikamano, watendee watu haki,
Waswihi maridhiano, basi mwogope Razaki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Kizazi hiki maono, gizani hakikaliki,
Twahoji mtafutano, na kulea wanafiki,
Twalitaka tangamano, hatutaki mamluki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Fanyeni mahojiano, na mengine mhakiki,
Hili la maelewano, dai letu, yetu haki,
Ni udhaifu utengano,milele hatuutaki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Umeisha mchuano, vizingiti na visiki,
Yatajiri mapatano, na mseto kuafiki,
Uongozi mlingano, lengo letu la twariki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Fursa zetu mshono, lakini nyuma twabaki,
Kichinichini mapigano, wengine wanatuhiliki,
Haishi misiguano, nchi haitajiriki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Farouk nawe Machano,vingine hatuimariki,
Tushikaneni mikono, na Mola atatubariki,
Mradi maelewano, tutahimili mikiki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Hatukulala kipono, kuwa tena hatuamki,
Tumeona mabishano, na njia isiyo milki,
Na ukweli ni uwiano, wananchi wastahiki,
Nena kilicho ukweli, vitendo viwe adili.

Wao wakipenda chao

Kwangu hilo sio tao, wala sio tegemeo,
Sio kama vipepeo, kwa mruko warukao,
Wala kwa rangi zao, na hizo safari zao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Nakusihi Samao, wewe mwenye milikiyo,
Nipe lako hifadhio, kwa dini niabuduyo,
Njia yangu lako chaguo, na wanangu wafuatao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Kwetu wewe kimbilio, kwa yote tutakayo,
Hukishi matarajio, kutupa yatufaayo,
Yaize matamaniyo, manufaa yasiyo nayo,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Hatuziwezi mbio zao, na mizigo wabebayo,
Na tukiwafuata wao, sio kati ututumayo,
Tunashika amriyo, hatuzishiki za kwao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Wache wapende wa kwao, hao wajidhaniao,
Wa kwetu si wa kwao, hao leo wawajuao,
Na wa kwetu uzao, ni wewe uwapendao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Wajinga ni waliwao, kwa wasiojua wao,
Upendo si mafao, wala chuki sio kilio,
Hutaka uyatakayo, hutumia upewayo,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Dua yangu mapitio, kwa wale niwafaao,
Thawabu wape wajao, pamoja na kinga yao
Ukirimu huu uzao, kuijua dini yao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Nimefikia kituo, na ujumbe ndio huo,
Wale mzingatiao, yawafae marejeo,
Wasiponifaa wao, utanipa unipao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !

Maajidi ni wanao, hawa tukuachiao,
Waongoze upendavyo, uwe mwema mwisho wao,
Wape lako kusudio, ndiwe uwajengao,
Wao wakipenda chao, Badi penda kilo changu !